Azimio 2371 ni ujumbe dhahiri kwa DPRK kuwajibika kwa amani na usalama:Guterres

16 Agosti 2017

Kuna zahama nyingi hivi sasa duniani kote, hasa mvutano kuhusiana na rasi ya Korea ambao haujashuhudia katika kiwango hicho kwa miongo. Hayo yamesema leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alipozungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya umoja wa Mataifa New York Marekani.

Amesema historia inakumbusha machungu ya miaka zaidi ya 67 iliyopita ya vita vya Korea ambapo zaidi ya watu milioni tatu walipoteza maisha idadi kubwa kuliko hata vita vya pili vya dunia , na kusisitiza kwamba dunia yapaswa kujifunza na kutorejea makosa kwa kuheshimu azimio la baraza la usalama nambari 2371.

(SAUTI YA GUTERRES)

“Azimio linatuma ujumbe usio na utata kuhusu wajibu wa amani na usalama kwa Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea. Na natoa wito kwa nchi zote wanachama Lakini pande zote husika lazima zitambue kwamba kupitishwa kwa kauli moja kwa azimio 2371 kunatoa fursa ya kutatua mgogoro huu kupitia diplomasia na kufufua majadiliano ya kutatua mzozo huu.”

Ameongeza kuwa suluhu ni lazima iwe ya kisiasa kwani uwezekano wa athari za kutumia suluhu ya kivita hata hazielezeki.

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres: Picha: UN Photo/Mark Garten

Kuhusu hali inayoendelea nchini Venezuela Katibu Mkuu amesema nchi za Amerika ya Kusini zimejitahidi kuachana na kuingiliwa na misimamo toka nje na utawala wa mkono wa chuma, lazima walinde hali hiyo, na kwa mukhtada huo(SAUTI YA GUTERRES VENEZUELA)

“Ujumbe ni bayana kwamba Venezuela inahitaji suluhu ya kisiasa kwa njia ya majadiliano na muafaka baina ya serikali na upinzani. Natambua juhudi za wapatanishi wa kimataifa na viongozi wa kikanda, naunga mkono juhudi hizo na nina waasa serikali na upinzani kuanza majadiliano kwa sababu naamini kwamba suluhisho pekee ni suluhisho la kisiasa kutokana na majadiliano hayo"

image
Maandamano yaliyofanyika Charlottesville nchini Marekani. Picha: UM

Na alipoulizwa kuhusu suala la chuki na ubaguzi wa rangi lililozusha tafran huko Charloteville mchini Marekani Katibu Mkuu amesema(SAUTI YA GUTERRES USA)

“Misingi ninayosimamia ni bayana , ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni , chuki dhidi ya wayahudi na waislamu unatia sumu jamii zetu, na ni muhimu sana kwetu sote kusimama kidete kupinga vikali kila mahali na kila wakati"