Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uharibifu wa silaha umekamilika katika kambi za FARC-Arnault

Uharibifu wa silaha umekamilika katika kambi za FARC-Arnault

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Colombia, Jean Arnault amesema amefurahishwa na operesheni za kusalimisha silaha nchini humo.

Katika taarifa yake ya Agosti 15, bwana Arnault amesema mchakato wa kuondoa silaha zote na risasi katika kambi 26 za kikundi cha FARC umekamilika. Ameongeza kwamba kando na operesheni ambayo inaendeshwa eneo Pondores lakini pia harakati zinaendelea katika maeneo mengine manne ikiwemo: La Reforma, Yari, La Guajira na La Variante.

Kufikia sasa amesema uharibifu wa silaha kutoka kambi zote 26, ikiwemo vilipuzi na mabomu ya kutega ardhini umekamilika.

Bwana Arnault ameongeza kwamba

(Sauti ya Arnault)

"Uharibifu wa idadi kubwa ya silaha hizo ni ishara ya mchakato mkubwa wa kutokomeza silaha sio tu kutoka kwa watu binafsi bali pia kuhakikisha uharibifu wa silaha zote chini ya FARC na kama alivyosema rais Juan Manuel Santos wa Colombia, hii inasogeza nchi katika hatua mpya."

Kwa upande wake Rais Santos amesema,

(Sauti ya Manuel Santos)

"Ningependa kuchukua nafasi hii kumshukuru bwana Arnault na wanachama wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwa kazi kubwa waliyofanya na pia kwa viongozi serikalini na kwa wanachama wa kundi la FARC kwa sababu hii imekuwa ni juhudi kutoka kwa wote. ni juhudi zilizozaa matunda. Licha ya kwamba kulikuwa na vikwazo na muda uliowekwa haukutimizwa miezi minane tangu kutiwa saini mkataba wa amani hatimaye mchakato wa kusalimisha silaha umefikiwa. Mchakato huu ukilinganishwa na mingine umeshikilia rekodi. Ireland Kaskazini walichukua miaka kumi , Colombia ni miezi minane tu."