Tuna deni na kizazi kijacho kutoa msaada wa kibinadamu leo:O’Brien

16 Agosti 2017

Kutoa usaidizi wa kibinadamu unaohitajika leo hii , ni uwekezaji wenye amana kubwa katika kizazi kijacho. Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa operesheni za misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien katika kuelekea siku ya usaidizi wa kiutu duniani itakayoadhimishwa Agosti 19.

Mwaka huu siku hiyo inajikita katika mashambulizi dhidi ya raia na wahudumu wa kibinadamu katika maeneo yenye mizozo duniani, kwamba sio walenga ikienda sanjari na kampeni ya #NotAtarget.

Kampeni hiyo inatanabaisha watu waliojikuta katikati ya machafuko ambayo hawakuyaanzisha, na inatoa wito wa ulinzi zaidi kwa wahudumu wa afya ambao wamekuwa wakilengwa kwa makusudi katika maeneo kama Syria na Yemen.

O’Brien amesema alishuhudia jukumu la wahudumu wa kibinadamu Yemen alipozuru shule inayohifadhi wakimbizi na wandani na kukutana na watoto tisa waliopoteza wazazi wao wote wawili..

(O’BRIEN CUT)

“Kulikuwa na msichana anaitwa Mari alikuwa anawaangalia wadogo zake wanane bila kuwa na wazazi na walikuwa wakihangaika kupata chakula na hatimaye waliandikishwa na kuanza kupata msaada kutoka kwa wahudumu wa misaada wenye ujasiri kutoka Umoja wa Mataifa, mashirika mingine yasiyo ya kiserikali ya kitaifa na kimataifa, hivyo waliweza kupata chakula na kwa kiasi fulani huduma za afya..”

Hata hivyo ameongeza..

(O’BRIEN CUT- 2)

“Haikuwa rahisi wao kupata huduma ya shule, na hilo lilinigusa kuliko kitu kingine chochote kwani hawapaswi kuwa wahanga katika vita vya watu wengine na walikuwa wakihangaika sana, lakini jumuiya ya kimataifa ilikuwa inafanya kazi nzuri kuhakikisha inawapa msaada wa kuokoa maisha pamoja na ulinzi waliokuwa wakiuhitaji.”