Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mipango ya kikosi cha G5 ilandane na mchakato wa amani Mali- Wane

Mipango ya kikosi cha G5 ilandane na mchakato wa amani Mali- Wane

Kadri hali ya usalama inavyozidi kuzorota kwenye mipaka ya nchi zilizo ukanda wa Sahel, Afrika Magharibi, ndivyo umuhimu wa kikosi cha pamoja cha nchi tano kwenye ukanda huo kinavyozidi kupata umuhimu.

Hiyo ni kwa mujibu wa Naibu Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa El-Ghassim Wane wakati akipatia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani taarifa za utekelezaji wa azimio namba 2359 la mwaka lililopitishwa miezi miwili iliyopita kuridhia kuanzishwa kwa kikosi hicho.

Ametolea mfano mashambulizi nchini Mali na kuzidi kupungua kwa idadi ya wafanyakazi wa serikali kwenye maeneo ya kaskazini kwa hofu ya usalama wao akisema tangu mwaka jana asilimia 10 ya wafanyakazi wa umma wameondoka maeneo hayo na huduma zinadorora.

Bwana Wane amesema hatua zimechukuliwa kwa kikosi hicho cha pamoja kuanza kazi ikiwemo kuchangisha fedha, hadi sasa asilimia 25 ya dola milioni zaidi ya 490 zinazohitajika zimepatikana.

Amesema mchakato unaendelea ili kikosi kianze operesheni zake mwakani lakini..

(Sauti ya Wane)

“Ningependa kusisitiza umuhimu wa kuzingatia siasa na mkakati wa kisiasa katika kuongoza shughuli za kikosi hicho cha pamoja ili kuhakikisha kuwa ziko sanjari na mchakato wa amani wa Mali na mipango mingine ya kikanda.”

Nchi zinazounda G5 kwenye ukanda wa Sahel ni  Mauritania, Mali, Burkina Faso, Niger na Chad.