Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya iko katika wakati muhimu, viongozi wawajibike-Zeid

Kenya iko katika wakati muhimu, viongozi wawajibike-Zeid

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amepongeza wananchi wa Kenya kwa kushiriki uchaguzi mkuu kwa njia ya amani huku akihimiza viongozi wa kisiasa kuwajibika na kuonyesha uongozi imara ili kuzuia machafuko zaidi.

Zeid ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti za vyombo vya usalama kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji na ripoti za ukatili wa polisi uliosababisha maafa na majeraha, ikiwemo kwa watoto. Maandamano yalizuka baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi Agosti 11, ambapo baadhi ya watu walianza kurusha mawe, kupora na kuharibu mali.

Hatahivyo, amesema watu wana haki ya kuandamana kwa njia ya amani na mamlaka lazima ichukue wajibu wa kuwalinda na serikali kuhakikisha vyombo vya usalama vinatoa kipaumbele kwa mazungumzo, na njia zingine za amani na kutumia nguvu tu wakati hakuna njia mbadala.

Aidha ameelezea kusikitishwa kwake na maamuzi ya bodi ya vyama visivyo vya serikali kutangaza kufungwa kwa shirika la African Centre for Open Governance na kukamatwa kwa wakurugenzi na wanachama wake.

Zeid pia ametoa wito kwa vyama vya umma na wanahabari kuruhusiwa kufanya kazi bila vikwazo au uoga.