Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maporomoko ya udongo Sierra Leone, juhudi za uokozi zaendelea

Maporomoko ya udongo Sierra Leone, juhudi za uokozi zaendelea

Nchini Sierra Leone, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanashirikiana na serikali kupeleka huduma za uokoaji kwenye maeneo yaliyokumbwa na maporomoko ya udongo na mafuriko mapema jana Jumatatu.

Zahma hiyo imekumba mji wa Regent na mji mkuu Freetown ambapo kupitia ukurasa wake wa Twitter, shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF linasema wanahaha kunasua familia kutoka kwenye matope.

Nalo shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM tayari limetoa dola 150,000 ili kusaidia harakati za dharura za uokoaji kwenye janga hilo linaloripotiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200.

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa taarifa kuelezea masikitiko yake juu ya tukio hilo akisema Umoja wa Mataifa uko bega kwa bega katika juhudi za uokoaji.