Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 7.7 wahitaji msaada wa haraka DRC: FAO/WFP

Watu milioni 7.7 wahitaji msaada wa haraka DRC: FAO/WFP

Wakati machafuko na watu kutawanywa kukiendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC , watu milioni 7.7 wanakabiliwa na njaa kubwa yameonya mashirika ya Umoja wa Mataifa, la chakula na kilimo FAO na la mpango wa chakula duniani WFP. Flora Nducha na taarifa kamili

(FLORA TAARIFA)

Katika ripoti yao mpya iliyotolewa leo mashirika hayo yanasema hilo ni ongezeko la asilimia 30 katika kipindi cha mwaka mmoja . Ripoti hiyo inayotathimini hali ya uhakika wa chakula (IPC) imetaja kati ya Juni 2016 na Juni 2017 , idadi kubwa ya watu walio katika dharura ya kutokuwa na uhakika wa chakula daraja la 4 na la 3 linalokaribia baa la njaa na kuhitaji msaada wa haraka wa chakula, imeongezeka kwa watu milioni 1.8. kutoka milioni 5.9 na kufikia watu milioni 7.97.

FAO na WFP wanasema zaidi ya mtu mmoja kati ya 10 wanaoishi vijijini wanakabiliwa na njaa ya kupindukia. Hali hii imechangiwa na machafuko yanayoendelea katika majimbo ya Kasai na Tanganyika ambako watu zaidi ya milioni 1.4 wamelazimika kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao. Miongoni mwao ni Bi Agness Lupetu aliyelazimika kuwa mkimbizi wa ndani baada ya kupoteza watoto wake wote sita na kusalia na majeraha ya moto

(AGNES CUT)

"Watoto wangu sita walichomwa moto wakiwa hai nyumbani kwangu, mume wangu alikimbia sijui kama yuko hai au amekufa. Nilipatiwa matibabu ya kienyeji Kamoina . Nyumba yangu ilichomwa moto na wanamgambo , sielewi ni jinsi gani niliweza kutoroka , nilitumia siku mbili msituni bila matibabu..”