Nitapaza sauti za vijana- Jayathma

12 Agosti 2017

Umoja wa Mataifa uko pamoja nanyi na mimi mjumbe wenu, nitafanya kila niwezalo kuhakikisha sauti zenu zinasikika.

Huo ni ujumbe wa mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu maswala ya vijana, Jayathma Wickramanayake akizungumza katika hafla ya kuadhimisha siku ya vijana duniani leo Agosti 12 iliyofanyika nchini Iraq.

Kauli  mbiu ya siku hii ikiwa "Vijana kujenga amani”, Bi. Wickramanayake amesema maelfu ya vijana wasichana na wavulana hufanya kazi kwa bidii, na mara nyingi katika mazingira hatarishi bila msaada au kuenziwa, katika juhudi za kujenga amani na kuimarisha usalama kwa wote. 

Mwakilishi huyo akizungumzia Iraq amesema, kama nchi yenye idadi kubwa zaidi ya vijana kote ulimwenguni huku takriban asilimia 50 ya raia wakiwa chini ya umri wa miaka 19, Iraq iko katika nafasi ya kuwezesha kundi hilo katika kuchagiza amani na maendeleo.

Hafla hiyo iliyoratibiwa kwa ushirikiano na ofisi ya  shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA nchini Iraq, ilileta pamoja vijana kutoka kona zote za nchi pamoja na viongozi wa serikali ikiwemo waziri wa vijana na michezo na mratibu wa usaidizi wa kibinadamu nchini Iraq Lise Grande.

Hii ni hafla ya kwanza ya bi. Wickramanayake tangu alipoteuliwa kuchuka nafasi ya mwakilishi maswala ya vijana.