Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama laitandika vikwazo vigumu DPRK:

Baraza la usalama laitandika vikwazo vigumu DPRK:

image
Wajumbe wa baraza la Usalama la UM wakipiga kura. Picha na UMBaraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo kwa kauli moja limepiga kura na kupitisha azimio nambari 2371 la kuongeza vikwazo kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea au DPRK.

Wajumbe wote 15 wa baraza wamepitisha azimio hilo linaloizuia DPRK kusafirisha nje bidhaa kama makaa ya mawe, chuma cha pua , risasi na bidhaa za baharini kama samaki.

Pia linazizuia nchi kutoingia mikataba au ushirika wowote wa kifedha na watu binafsi au mashirika kutoka DPRK miongoni mwa masharti ya azimio hilo.

Mswada wa azimio hilo uliwasilishwa na Marekani , balozi wake kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley anasema ni azimio imara na ni hatua ya pamoja.

(HALEY CUT)

"Vitendo vya kutowajibika vya Korea ya Kaskazini na kutojali kwake vimeuponza utawala wa nchi hiyo kulipa gharama kubwa. Azimio hili ni kubwa la vikwazo vya kiuchumi kuwahi kuwekwa dhidi ya utawala wa Korea Kaskazini. Gharama ambazo uongozi wa Korea Kaskazini utalipa kwa kuendelea kuunda nyuklia na makombora itakuwa ni kupoteza theluthi moja ya bidhaa zake inazosafirisha nje na kuporomoka kwa sarafu yake. Hivi ni vikwazo vigumu Zaidi kwa nchi hoyote katika kizazi hiki.”

Baraza la usalama pia limesikitishwa kwamba DPRK imeelekeza rasilimali zake chache kwa mipango ya nyuklia. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA zaidi ya nusu ya watu wa DPRK wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula na huduma za afya.