Hali nchini yemen bado ni tete:UNDP

1 Agosti 2017

Hali nchini Yemen bado ni tete na inahitaji kuendelea kutupiwa jicho zaidi. Hayo ni kwa mujibu wa Auke Lootsma mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP nchini Yemen alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York kwa njia ya video.

Bwana Lootsma amesema hivi sasa Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba watu milioni 20 wanahitaji msaada wa kibinadamu ikiwa ni sawa na asilimia 70 ya watu nchini humo na kuongeza kwamba

(SAUTI YA LOOTSMA)

“Yemen imeingia katika mwaka wa tatu wa vita na licha ya juhudi za mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo hakuna dalili ya kumalizika kwa vita. Wakati huohuo ni dhahiri kwamba suluhu pekee ya mgogoro ni ya kisiasa, na kwa sasa watu wa yemen wanakabiliwa na madhila makubwa yakusikitisha.”

Bwana Lootsma ameitaka jumuiya ya kimataifa kuungalia kwa karibu mgogoro huo na kujitahidi kuupatia ufumbuzi ili kulinusuru taifa hilo na watu wake.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud