Afisa wa haki za binadamu Gilmour kuzuru Liberia

31 Julai 2017

Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu haki za binadamu, Andrew Gilmour, atazuru Liberia kuanzia Agosti Mosi hadi 3 katika jitihada za kutafuta kuungwa mkono ili kuanzisha ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo baada ya mpango wa Umoja wa Mataifa UNMIL kufungwa rasmi Machi 2018.

Katika ziara hiyo bwana Gilmour atakutana na viongozi wa serikali na wawakilishi wa asasi za kiraia ili kujadili masuala muhimu ya haki za binadamu yanayoikabili nchini hiyo. Umoja wa Mataifa unasema wakati Liberia imepiga hatua kubwa tangu mkataba wa amani 2003 na kufurahia amani na usalama , bado kuna changamoto kubwa za haki za binadamu.

Wakati uchaguzi mkuu wa Rais na bunge ukitarajiwa Oktoba mwaka huu, Bwana Gilmour atahimiza wito wa Umoja wa Mataifa nchini humo wa kutaka wadau wote kushirikiana ili kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa wa amani, huru na wa wazi.

Pia atajadili na serikali na washirika wengine haja ya kufuatilia kwa karibu hali ya haki za binadamu kabla ya uchaguzi na kuhakikisha hatua muafaka zinachukuliwa ili kuepusha kuzuka kwa machafuko .

Makundi mengine atakayokutana nayo ni wawakilishi wa kidiplomasia, asasi za kiraia na Umoja wa Mataifa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter