Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu alaani jaribio la kombora DPRK:

Katibu Mkuu alaani jaribio la kombora DPRK:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani kurushwa tena kombora la masafa marefu lenye uwezekano wa kuvuka mipaka ya nchi lililofanywa na jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea au DPRK leo. Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Katibu Mkuu amesema kitendo hicho kwa mara nyingine ni ukiukaji wa maazimio ya baraza la usalama.

Ameongeza kuwa uongozi wa DPRK ni lazima utimize kikamilifu wajibu wake wa kimataifa na kufanya kazi pamoja na jumuiya ya kimataifa kutatua masuala tete kwenye rasi ya Korea. Katibu Mkuu amerejea wito wake kwa uongozi wa DPRK kutoa jibu kuhusu mapendekezo ya Jamhuri ya korea ya kuanzisha majadiliano hususani kwa majeshi yao ili kupunguza hatari, kutoelewana na mvutano.