Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walindeni watoto wahamiaji dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu-UM

Walindeni watoto wahamiaji dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu-UM

Nchi zimetakiwa na wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa kuongeza juhudi za kuwalinda watoto wahamiaji dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, kuuzwa na mifumo mingine ya unyanyasaji.

Wawakilishi maalumu Maria Grazia Giammarinaro na Maud de Boer-Buquicchio wametoa wito huo kwa ajili ya siku ya kimataifa ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu ambayo huadhimishwa kila mwaka Julai 30.

Wameonya kwamba watoto huathirika zaidi na vita na majanga na wale waliotenganishwa na familia zao wanakuwa katika hali ya hatari zaidi.

Mfumo wa sasa wa kuwalinda watoto wahamiaji unashindwa na kuwaacha wengi wao katika hatari ya biashara haramu ya binadamu, na mifumo mingine ya unyanyasaji.

Maria Grazia Giammarinaro ni mwakilishi maalumu kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu anasema

(MARIA CUT)

“Njia za kuweka mazingira yanayojali zaidi maslahi ya mtoto hazifanyi kazi ipasavyo.Katiba baadhi ya nchi hakuna uwezekano wa kuteua mlezi mtu ambaye anaweza kutambua na kulinda kweli maslahi ya mtoto. Mara nyingi hakuna mbinu za kubaini endapo kuna hatari kwa mtoto kuingizwa katika mtandao wa usafirishaji haramu.”

Wataalamu hao pia wamezikosoa nchi ambazo zinaendelea kuwafunga watoto wahamiaji na kuweka sera za kuwabana badala ya sera za kuwalinda watoto.