Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada ya kibinadamu Syria yafikia idadi ya chini kabisa: OCHA

Misaada ya kibinadamu Syria yafikia idadi ya chini kabisa: OCHA

Ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa jamii zisizojiweza kabisa nchini Syria uko katika kiwango cha chini kabisa umesema leo Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA Jens Laerke, mwezi Julai hakujakuwa na misafara ya mashirika yoyote ya misaada katika maeneo yanayozingirwa nchini humo , lakini pia katika maeneo ambayo ni vigumu kufikika msafara umekuwa mara moja tu kwa wiki.

Zaidi ya watu nusu milioni wanaishi katika maeneo 11 yanayozingirwa nchini Syria na kuna watu milioni nne walioko katika maeneo ambayo ni vigumu kufikika.

OCHA inasema misaada inaendelea kudondoshwa kwa njia ya anga katika eneo la Mashariki la Deir Ez Zour.

Hadi sasa mwezi huu wa Julai Umoja wa Mataifa na washirika wake wamefanikiwa kuwafikia theluthi moja tu ya watu milioni moja wanapaswa kupokea msaada.