Neno la wiki: Rehani na Dhamana
Katika neno la wiki hii leo tunaangazia maneno "Rehani" na "Dhamana" Mchambuzi wetu ni Nuhu Zuberi Bakari, ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa masuala ya mawasiliano kwenye Chama cha Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA.
Tukianza na Rehani, Bwana Zuberi anasema ukiwa na kitu ambacho unakipenda sana na unahitaji kukiweka rehani ili upate kitu kingine unachohitaji kama vile hela, inamaanisha kwamba utampelekea yule atakayekupa hela hizo kitu chako akiweke kisha unachukua hela, na utakapopata hizo hela unampelekea ili aweze kukurudishia kitu chako. Na tukiangalia neno "Dhamana" ina maana ya kwamba ukiwa na mtu unayemfahamu kama rafiki na anaomba kitu chochote akiwa na mpango wa kulipa baadaye, na mwenye anamuomba hamfahamu, ukijitolea kumsimamia hadi atapoweza kulipa basi wewe umemwekea dhamana au umesimama kama shahidi, kiwango cha kwamba hata asipoweza kukilipia wewe mwenyewe utakilipia.