Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na wadau waongeza kasi ya kudhibiti mlipuko wa surua Somalia

WHO na wadau waongeza kasi ya kudhibiti mlipuko wa surua Somalia

Somalia inakabiliwa na mlipuko mbaya kabisa wa surua katika kipindi cha miaka minne , limesema leo shirika la afya duniani WHO.

Ukame na tishio la baa la njaa ukiongezea na kiwango kidogo cha chanjo vimewaacha mamilioni ya watoto Somalia wakiwa dhaifu, wakikabiliwa na njaa na hususani hatari ya kukumbwa na mlipuko wa surua na maradhi mengine ya kutishia maisha.

WHO inasema takribani visa 14,000 vinavyoshukiwa kuwa surua vimeripotiwa mwaka huu pekee ukilinganisha na visa elfu tano hadi elfu kumi kwa mwaka tangu mwaka 2014.

Shirika hilo limeongeza kuwa asilimia 80 ya waliokumbwa na mlipuko wa sasa wa surua ni watoto wa chini ya umri wa miaka 10. Ili kudhibiti mlipuko huo na kupunguza idadi ya vifo miongoni mwa watoto kampeni ya nchi nzima ya chanjo ya surua itazinduliwa na WHO na shirika la kuhudumia watoto UNICEF, wakishirikisha wizara ya afya ya Somalia mwezi novemba mwaka huu, wakiwalenga watoto milioni 4.4 wenye umri wa kati ya miezi sita na miaka 10.