Raia takriban 50,000 wakwama Raqqa-Mueller

27 Julai 2017

Takriban raia 50,000 bado wamekwama katika eneo la Raqqa lililokuwa likidhibitiwa na kundi la kigaidi la Daesh, au ISIL, bila njia yoyote ya kujinasua.

Hayo yameelezwa na naibu msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu uratibu wa masuala ya kibinadamu (OCHA), alipohutubia baraza la usalama hii leo kuhusu hali nchini Syria.

Bi Ursula Mueller akizungunmza kwa niaba ya mratibu wa misaada ya binadamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien kwa njia ya video kutoka ofisi za OCHA mjini Amana Jordan, amesema kwa mujibu wa duru za habari muungano unaoungwa mkono na Marekani na wapiganaji wa Kiarabu wamefanikiwa kuyanyakuwa maeneo mengi ambayo kundi la kigaidi la Daesh lilijitangazia kuwa ni makao yake makuu.

Ingawa zaidi ya raia 200,000 wamefanikiwa kukimbia mapigano Bi Mueller amesema hali bado ni mbaya kwa waliokwama.

(SAUTI YA MUELLER 1)

"Watu wanaokadiriwa kuwa 20,000 hadi 50,000 wamesalia mjini Raqqa na hali yao iko njia panda hakuna jinsi yoyote ya wao kutoka nje. Raia kutoka nje ya mji huo bado ni vigumu sana kutokana na mabomu ya ardhini na vifaa vingine vya mlipuko, pamoja na uvurumishaji wa makombora, shughuli za walenga shabaha na mashambulizi ya anga.”

Na kuhusu mashambulizi yanayoendelea katika nchi jirani ya Iraq hususani mjini Mosul, amesema wapiganaji wa ISIL wamekuwa wakiwatumia raia mateka kama ngao. Pia ameongeza kuwa maisha ya kila siku ya Wasyria walio katika maeneo yaliyozingirwa au vijijini yanaendelea kuwa ya hatari huku wakikosa fursa na ushirikiano wa serikali ya Syria, na makundi yenye silaha yakiwa kikwazo kwa juhudi za Umoja wa Mataifa za kutoa msaada wa kuokoa maisha.

(SAUTI YA MUELLER2)

“Hakujakuwa na msafara wa misaada kwa maeneo yaliyozingirwa mwezi Julai, ingawa misaada inayodondoshwa kwa njia ya anga mjini Der-er-zor imeendelea. Kuhusu misafara katika maeneo ambayo ni magumu kufikika , imepungua hadi msafara mmoja kwa wiki Julai.”

Ameongeza kuwa wahudumu wa misaada ya kibinadamu wamewafikia Wasyria milioni 8.5 kwa mwezi mmoja licha ya kuendelea kwa vita na kunyimwa fursa ya kuingia baadhi ya maeneo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter