Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amina Mohammed na Rais Kabila wajadili nafasi ya mwanamke DRC

Amina Mohammed na Rais Kabila wajadili nafasi ya mwanamke DRC

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed amehitimisha ziara nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC alikopata fursa ya kuzungumza na serikali, wanawake, wakimbizi na wadau wengine. Grace Kaneiya na taarifa zaidi.

(TAARIFA YA GRACE)

Baada ya kukutana na wanwake na asasi za kiraia Bi Mohammed alikutana na Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo na kusema mkutano wao ulijikita katika masuala yanayowakabili wanawake nchini humo, ukizingatia kwamba wao ndio wanaobeba gharama kubwa za vita.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye uwanja wa ndege wa Kinshasa amesema miongoni mwa masuala hayo ni ujumuishi wa wanawake katika uchumi na hasa sekta ya kilimo lakini pia katika mchakato wa kisiasa ambapo amesema wametiwa moyo kwa kiasi fulani

(SAUTI YA AMINA)

“Tumeridhishwa na daftari la wapiga kura ambapo tayari kuna idadi kubwa ya wanawake ambao wameshajiandikisha kupiga kura , na suala la amani ambapo pia wanawake ndio wanaobeba gharama kubwa hivyo tunataka kuona ni jinsi gani wanawake watashiriki zaidi katika upatanishi na katika uwekezaji ambao utaangalia suala la afya, na huduma ambazo wanazihitaji.”

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa bado unahofia ukatili wa kijinsia unaoendelea nchini humo ingawa pia unatambua hatua zilizopigwa na zinazohitajika kuutokomeza. Na kuhusu suala la wataalamu wawili wa Umoja wa mataifa waliouawa kikatili nchini humo Bi Mohammed amesema

(SAUTI YA AMINA)

“Tulilizungumza hilo kwa Rais na akatuhakikishia kwamba watafuatilia chunguzi zinazofanyika haraka iwezekanavyo"

Na kituo cha mwisho kwa Bi Mohammed kabla ya kuondoka kilikuwa ni kambi ya wakimbizi wa ndani ya Mungunga inayohifadhi zaidi wanawake na watoto na kusema

(SAUTI YA AMINA)

"Ni lazima tupeleke sauti ya Kivu Kaskazini na ya kambi hii kwenye jumuiya ya kimataifa, hawa ni wanawake wetu wa Afrika na lazima tupeleke sauti yao nje, kwamba wanateseka na kwa mateso haya lazima tulete rasilimali sio kama msaada lakini kama haki ya msingi ya binadamu."