Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa kipindupindu Yemen; ni janga juu ya janga-UM

Mlipuko wa kipindupindu Yemen; ni janga juu ya janga-UM

Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa wamezuru Yemen kwa ajili ya kutathmini hali halisi ya janga la kibinadamu nchini humo na kuimarisha juhudi za pamoja kwa ajili ya kusaidi wananachi wa taifa hilo.

Wakuu hao wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, la mpango wa chakula duniani, WFP na Shirika la afya ulimwenguni, WHO katika taarifa yao ya pamoja wamesema kwamba mlipuko wa kipindupindu Yemen ndio mbaya zaidi kuwahi kutokea katika janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani.

Taarifa ya pamoja inasema kwamba katika kipindi cha miezi mitatu pekee, kumekuwa na visa laki nne na takriban vifo 1,900 kutokana na ugonjwa huo. Huduma muhimu ya afya, maji na huduma ya kujisafi zimesambaratishwa kufuatia mzozo wa miaka miwili na kusababisha mazingira yanayochochea ugonjwa kusambaa

Kwa mujibu wa Mashirika hayo, Yemen iko katika hatari ya kukumbwa na njaa, huku zaidi ya asilimia 60 ya watu hawajui mlo wao unakotoka. Aidha takriban watoto milioni mbili waYemeni wanaugua utapiamlo uliokithiri hali ambayo inawaweka katika hatari ya kuambukizwa kipindupindu na magonjwa yanayochagiza utapiamlo na hivyo kuwaweka katika msururu wa matatizo.