Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauji ya walinda amani wengine wawili CAR yalaaniwa:UM

Mauji ya walinda amani wengine wawili CAR yalaaniwa:UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amelaani vikali mauaji ya walinda amani wengine wawili nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Mauji hayo ya walinda amani kutoka Morocco wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini CAR , MINUSCA yaliyotokea jana mjini Bangassou yanafanya idadi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliouawa nchini humo tangu mwanzo wa mwaka kufikia tisa.

Kupitia taarifa ya msemaji wake, Guterres aliyetuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika , watu na serikali ya Morocco na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi, ameitaka serikali ya CAR kuchunguza mauaji hayo na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria.

Katibu Mkuu amesema anatiwa hofu na hali ya mvutano inayoendelea Kusini Mashariki mwa nchi, akionya kwamba hali hiyo ikiruhusiwa kuendelea itazototesha mafanikio yaliyofikiwa ya mchakato wa kuelekea amani ya kudumu.

Ametoa wito kwa pande zote katika mzozo kukomesha machafuko na kuchukua hatua ya kuepuka kuzorotesha zaidi hali ya usalama katika taifa hilo.