Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matatizo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria yatokana na maendeleo duni: UNDP

Matatizo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria yatokana na maendeleo duni: UNDP

Matatizo ya Kaskazini Mashariki mwa Nigeria kimsingi yanatokana na changamoto za maendeleo duni zilizochangiwa na uasi wa kundi la kigaidi la Boko Haram ambao umesababisha mgogoro wa kiwango cha kimataifa.

Huo ni mtazamo wa mwakilishi na mratibu mkazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP nchini Nigeria , Edward Kallon. Karibu Wanaigeria milioni mbili wamekuwa wakimbizi wa ndani, huku wengine kwa maelfu wakilazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger; nchi ambazo pia zina matatizo.

Wanigeria wengine takribani milioni 8.5 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu na machafuko ya Boko Haramu yamekatili maisha ya watu wapatao 20,000 hadi sasa. Lakini Bwana Kallon anasema mgogoro huo uonekane kama fursa ya kurekebisha miongo ya upungufu wa maemndeleo

(KALLON CUT)

“Ni fursa kwa maana ya kujaribu kwa mara nyingine kuangalia chanzo cha mgogoro, ambachi ni mapungufu ya maendeleo, utawala, mapungufu katika haki za binadamu, umasikini na changamoto za hali ya hewa.”

Akifafanua kuhusu mikakati ya UNDP amesema

(KALLON CUT 2)

“Mpango wa maendeleo wa Umoja wa mataifa ulikuja hapa kuwa draja la mpito kutoka msaada wa kibinadamu , kuelekea kujikwamua na maendeleo ya muda mrefu. Tunahitaji amani, tunahitaji suluhu ya uasi wa Boko Haram na pia tunahitaji mchakato wa kisiasa iki kusaidia juhudi za kijeshi kusaka suluhu ya kudumu.”