Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko Jerusalem yana athari zaidi ya Mashariki ya Kati:Mladenov

Machafuko Jerusalem yana athari zaidi ya Mashariki ya Kati:Mladenov

Machafuko yanayoendelea kwenye mji wa kale wa Jerusalem yana athari kubwa sio kwa Israel au Palestina pekee bali ni kwa dunia nzima.

Hayo yamesemwa na mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati bwana Nickolay Mladenov katika mjadala maalumu kuhusu hali ya Mashariki ya Kati uliofanyika leo kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, New York Marekani.

Akizungumzia machafuko na mvutano ulioshika kasi ndani na maeneno yanayozunguka mji mtakatifu wa kale wa Jerusalem baada ya majeshi ya Israel kuanza kuweka vifaa vya ukaguzi na kamera na kuchukua hatua zingine za kiusalama kwenye msikiti wa Al Aqsa , Mladenov amesema machafuko hayo yanaweza kuwa janga kubwa litakalogharimu zaidi ya kuta za mji mkongwe.

(MLADENOV CUT)

"Mtu yeyote asihamanike kuwa matukio haya ni ya eneo husika tu,ukweli ni kwamba huenda yanatokea katika mamia ya mita tu lakini yanaathiri mamilioni kama sio mabilioni ya watu duniani kote, yana uwezekano wa kuwa janga la gharama kubwa zaidi ya kuta za mji wa zamani, zaidi ya Israel na Palestina na zaidi ya Mashariki ya Kati .”

Mladenon pia amewataka wajumbe wa baraza la usalama kutumia ushawishi wao kwa kila upande ili kuwachagiza kusitisha machafuko na kuhakikisha kwamba wakati ulinzi unatolewa kwa waumini na wageni kwenye maeneo matakatifu mjini Jerusalem, hali ambayo imeanzishwa tangu mwaka 1967 inalindwa, kuheshimiwa na kuhifadhiwa kwa wote.