Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yazinduaa mkakati mpya Tanzania kwa ajili ya SDG’s

WFP yazinduaa mkakati mpya Tanzania kwa ajili ya SDG’s

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limezindua mkakati wa miaka mine wa kitaifa nchini Tanzania (CSP). Mkakati huo unakwenda sanjari na ajenda ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu kwa lengo la kutokomeza umasikini, kupunguza pengo la kutokuwepo usawa, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuhakikisha kilimo endelevu na uhakika wa chakula.

Kwa mujibu wa WFP mkakati huo unalenga kuboresha fursa ya masoko kwa wakulima wadogowadogo 250,000, huku ikizingatia pia programu inayohusisha sekta mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha lishe kwa kina mama wajawazito na wanaonyonyesha wapatao 185,000. Pia utajumuisha lishe ya watoto walio chini ya umri wa miaka miwili na kutoa msaada wa chakula kwa wakimbizi zaidi ya laki tatu.

Mkakati huo wa CSP utatoa fursa kwa serikali ya Tanzania kubaini maeneo ya kuyapa kipaumbele na kwa ushirika na wadau WFP itaweza kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa jamii zisizojiweza kuhimili mabadiliko na kuwa na uhakika wa chakula.

Mkakati huo wa CSP umeandaliwa ili kuwezesha mipango ya muda mrefu ya usaidizi wa Umoja wa Mataifa na uliandaliwa kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania, wahisani na wadau wengine wa maendeleo.