Wahusika wa shambulio la kigaidi Lahore wawajibishwe:Guterres
Wahusika wa shambulio la kigaidi lililofanyika leo mjini Lahore, Pakistan lazima wawajibishwe. Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa ya msemaji wake akilaani vikali shambulio hilo.
Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika na kuwatakia ahuweni ya haraka wajeruhi.
Takribani watu 26 wameuawa katika shambulio hilo la kigaidi na wengine wengi kujeruhiwa.
Katibu Mkuu amesema anaunga mkono juhudi za serikali ya Pakistan za kupambana na ugaidi na ghasia za itikadi kali, kwa kuheshimu misingi ya kimataifa ya haki za binadamu na wajibu wake.