Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya usalama na haki za binadamu inaendelea kudorora Mynmar- Mtaalam

Hali ya usalama na haki za binadamu inaendelea kudorora Mynmar- Mtaalam

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu ametoa ripoti inayoshtumu serikali ya Mynmar kuendeleza sera zinazofanana na zile za serikali ya kijeshi ya awali na kudumisha hali mbaya zaidi ya kiusalama na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Yanghee Lee akitoa ripoti yake kufuatia ziara ya siku kumi na mbili nchini Mynmar ameelezea kusikitishwa kwake kufuatia ripoti za mauaji, unyanyasaji, kutumika kwa watu kama ngao na vyombo vya usalama, maafa vizuizini na janga la kibinadamu la watu wa Rohingya na watu wa makundi mengine madogo madogo ambao wamelazimika kukimbia makwao.

Mtaalam huyo ambaye alizuru maeneo ya Yangon na Nay Pyi Taw na maeneo ya majimbo ya Rakhine, Shan na Kayin amesema ziara yake ilidhibitiwa kwa kiasi kikubwa na ufikiaji wa maeneo kunakoshuhudiwa majanga kunaudhibiti dhidi ya mashirika ya kimataifa huku watu waliokutana naye wakikabiliwa na unyanyasaji.

Aidha Bi. Lee ameelezea hofu yake kuhusu kunyakuliwa kwa ardhi kwa ajili ya kutenga maeneo maalum ya kiuchumi bila kuwafidia wakulima na jamii za wavuvi huku juhudi za marekebisho zikigonga mwamba kwani wanalazimika kulipia ardhi hizo kodi au kuzinunua upya kwa bei ya juu zaidi.

Katika ziara yake ya kati ya Julai 10-21 kwa mwaliko wa serikali ya Mynmar, mtaalamu huyo amekutana na maafisa wa serikali, viongozi wa jamii, wawakilishi wa vyama vya umma na wahanga wa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Bi Lee, atawsilisha ripoti kamili kwa baraza kuu la Umoja wa Mataifa Oktoba 2017.