Zaidi ya watu 20 wauawa katika shambulio, UNAMA yalaani vikali

24 Julai 2017

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA, umelaani vikali shambulio la kujitoa muhanga lililotokea leo mjini Kabul, wakati nchi nzima ikiwa katika hali ya taharuki kutokana namachafuko yanayoathiri raia kwa kiasi kikubwa.

Shambulio hilo la leo asubuhi limekuja wakati watu wakiadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja ya shambulio la 23 Julai 2016 kwenye uwanja wa Dehmazang lililokatilia na kujeruhi mamia ya waandamanaji walikuwa wakitekeleza haki yao ya uhuru wa kukusanyika na kujieleza.

Abiria na wapita njia zaidi ya 20 wameuawa kwenye shambulio la leo wakati mshambuliaji wa kujitoa muhanga alipolipua gari lililosheheni vilipuzi karibu na basi lililokuwa limejaa watumishi wa umma kwenye eneo la Ghulayee Dawa mjini Kabul watu wengine zaidi ya 40 wamejeruhiwa.

Kundi la kigaidi la Taliban limedai kuhusika na shambulio hilo. Pernille Kardel naibu mwakilishi wa Katibu Mkuu na kaimu mkuu wa UNAMA amesema amesikitishwa sana na shambulio hilo dhidi ya raia , na kuliita ni la kiuoga na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa UNAMA mashambulizi ya kujitoa muhanga yanayotekelezwa na wapinga serikali ndio chanzo kikubwa cha vifo vya raia na majeruhi nchini Afghanistan kwa mwaka 2017.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter