Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nini mchango wa wahamiaji wa ughaibuni kwa SDG’s:IOM

Nini mchango wa wahamiaji wa ughaibuni kwa SDG’s:IOM

Wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa , mashirika ya Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia, wahamiaji na viongozi wa wahamiaji ughaibuni wanakutana hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa leo na kesho kujadili suala la wahamiaji. Amina Hassan na taarifa kamili

(TAARIFA YA AMINA)

Majadiliano hayo ni ya nne ya mchakato wa nchi wanachama wa kuanzisha mkakati wa kimataifa kwa ajili ya usalama, mpangilio na usaidizi wa wahamiaji (GCM).

Mada kuu ya mjadala huo ni “Mchango wa wahamiaji na walio ughaibuni katika nyanja zote za maendeleo endelevu ikiwemo utumaji fedha nyumbani na faida wanazozipata”.

Mkutano huo pia utathimini changamoto na fursa katika uchumi na jamii zinazochangiwa na wahamiaji katika nchi wanazotoka na wanakoishi mfano kuleta elimu na ujuzi. Akizungumza katika mjadala huo Louise Arbour katibu mkuu wa mkutano huo wa kimataifa amesema

(Sauti ya Louise Arbour)

"Dola bilioni 429 zilizotumwa katika nchi zinazoendelea mwaka 2016 ni moja ya mchango mkubwa unaoonekana wa wahamiaji wa kuweza kufikia malengo ya maendeleo endelevu kwa nchi walikotoka, ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya msaada rasmi wa kimataifa wa maendeleo. fedha hizo kwa nchi zinazoendelea zimewatoa mamilioni ya familia kutoka kwenye umasikini."

Na kwa nchi waliko ameongeza

(Sauti ya Louise Arbour)

"Kwa ujumla wahamiaji wana mchango mkubwa wa maendeleo kwa nchi waliko, hususani mchango wa nguvu kazi, katika viwango vyote vya ujuzi, na hili ni muhimu tukalizingatia kwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea, wahamiaji huziba pengo la ajira ambazo hazijazwi na wenyeji na kuruhusu uchumi kukua kwa haraka."