Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani mauaji ya mlinda amani wa MINUSCA:

Guterres alaani mauaji ya mlinda amani wa MINUSCA:

Mauaji ya mlinda amani wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, yaliyotokea jumapili yamelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Guterres amesema mauaji hayo yanashukiwa kufanywa na mwanamgambo wa anti-Balaka mjini Bangassou, Kusini Mashariki mwa CAR ambapo watu wengine watatu walijeruhiwa.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia na serikali ya ufalme wa Morocco anakotoka mlinda amani huyo na pia kuwatakia afuweni ya haraka majerihi. Guterres amesema anasikitishwa na mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na kuitaka serikali ya CAR kuchunguza tukio hilo na kuwafikisha wahusika kwenye mkono wa sheria.

Pia amesema anatiwa hofu na kuendelea kwa mapigano Kusini Mashariki mwa nchi hiyo na kutoa wito kwa pande zote kupunguza ghasia. Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuisaidia MINUSCA kulinda raia na kusaidia kurejesha utulivu na usalama nchini CAR.