Papa Francis atoa mchango kwa FAO kusaidia watu wanaokabiliwa na njaa Afrika Mashariki

Papa Francis atoa mchango kwa FAO kusaidia watu wanaokabiliwa na njaa Afrika Mashariki

Katika hatua isiyo ya kawaida, papa mtakatifu Francis ametoa mchango wa euro 25,000 kwa ajili ya mipango ya Shirika la kilimo na chakula duniani FAO wa kuwasaidia watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula na ukame Afrika Mashariki.

Papa Francis amesema kwamba fedha hizo ni mchango wa mfano kwa ajili ya mradi wa FAO unaotoa pembejeo kwa familia zilizo vijijini katika maeneo yaliyoathiriwa na mizozo na ukame.

Ujumbe wa papa Francis uliowasilishwa kupitia barua kwa mkurugenzi mkuu wa FAO José Graziano da Silva unasema kwamba ishara hiyo ya papa Francis imetokana na ahadi aliyotoa katika kongamano la FAO mapema mwezi huu na ari ya kuchagiza serikali.

Ukame ulitangazwa nchini Sudan Kusini mwezi Februari na licha ya kwamba hali imeimarika kidogo baada ya misaada ya kibinadamu lakini watu milioni 6 nchini humo bado wanahaha kupata chakula toshelezi kila siku.

Aidha idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kibindamu katika nchi zingine tano Afrika Mashariki ikiwemo Somalia, Ethiopia, Kenya, Tanzania na Uganda inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 16 ambayo ni ongezeko la asilimia 30 tangu mwishoni mwa mwaka 2016.

Papa Francis anatarajiwa kushiriki maadhimisho ya siku ya chakula duniani mwezi Oktoba mwaka huu.