Je! Wahalifu dhidi ya Albino Tanzania wamehamia kwingine?

Je! Wahalifu dhidi ya Albino Tanzania wamehamia kwingine?

Ingawa visa vya mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania vinashuka, na hiyo ni habari njema, cha kushangaza ni kuwa visa hivyo vimepanda zaidi nchini Malawi na Msumbiji na sababu yake haijulikani.

Hilo ni kwa mujibu wa mtaaalamu huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Ikponwosa Ero, ambaye amealikwa kuzuru Tanzania tangu Julai 18-28, kufanya tathimini kuhusu hali ya watu wenye ulemavu wa ngozi au Albino, kubaini changamoto zilizopo na hatimaye kutoa mapendekezo.

Amesema hivi karibuni ripoti za mashambulizi alizopokea kutoka Tanzania zimeshuka mno..

(Sauti ya Ekiponwosa)

"Sijui kama kuna visa vya mashambulizi ambavyo havijaripotiwa, lakini katika visa vilivyoripotiwa idadi imeshuka, na hii ni habari njema, nipo hapa kuchunguza ni hatua zipi zimechukuliwa na kusababisha kushuka kwake, ili ziigwe katika nchi zingine ambazo tatizo hilo bado lipo. Na mwaka huu kila kisa nilichopokea cha ukiukwaji wa haki ya watu wenye ualbino, ni kutoka nje ya Tanzania."

Ameongeza kuwa kushuka kwa idadi ya uhalifu Tanzania na kupanda kwake kwa kasi Malawi na Msumbiji ni jambo la kutafakari kwani...

(Sauti ya Ekiponwosa 2)

"Unashangaa kama wahalifu ni walewale na au kama wamesukumwa nje ya Tanzania na sasa wamekwenda kufanya uhalifu kwingine, kuna maswali mengi kuliko majibu".

Bi Ero amezuru Mwanza na Dar-es-Salaam na ataelekea Kigoma na Dodoma katika ziara hiyo ambayo itamkutanisha pia na viongozi wa serikali, asasi za kiraia na wadau wote husika.