Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ninatiwa hofu na ongezeko la mvutano Jerusalem: Mladenov

Ninatiwa hofu na ongezeko la mvutano Jerusalem: Mladenov

Mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati leo amesema kwamba anatiwa hofu na kuongezeka kwa mvutano katika maeneo matakatifu ya mji wa kale wa Jerusalem.

Nickolay Mladenov ametoa taarifa akikaribisha hatua ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ya kujizuia na kuheshimu hadhi ya maeneo matakatifu ya mji huo. Pia amekaribisha hatua ya Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ya kulaani vikali machafuko hususan shambulio lililokatili maisha ya polisi wawili wa Israel Julai 14 Ijumaa iliyopita ambalo lililotokea katika lango kuu la kuingilia kwenye eneo la mji wa kale wa Jerusalem linalochukuliwa kama eneo takatifu kwa wote Wayahudi na Waislam.

Washambuliaji wote watatu waliuawa na majeshi ya Israel baada ya kufanya mashambulizi kwa kutumia bunduki na visu dhidi ya polisi.

Bwana Mladenov amesema anatumai taarifa zilizotolewa na viongozi wote wawili zitasaidia kutatua mvutano na kukomesha hali hiyo ambayo imeongeza chokochoko wiki iliyopita.