Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili dhidi ya watoto waongezeka CAR-UNICEF

Ukatili dhidi ya watoto waongezeka CAR-UNICEF

Visa vya ukatili dhidi ya watoto, ikiwemo ubakaji, kutekwa nyara mauaji na kusajiliwa watoto katika vikundi vilivyojihami, vimeongezeka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), sanjari na kuzuka upya kwa mapigano,  limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, kama atavyotujuza John Kibego katika ripoti ifuatayo.

(Taarifa ya John Kibego)

Shirika hilo limesema huenda visa vya ukatili dhidi ya watoto katika miezi mitatu iliopita, vikawa vingi kuliko ilivyoripotiwa, kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama na kukatishwa kwa shughuli za kibinadamu katika meoneo mengi.

Aidha, taarifa za UNICEF zinaonyesha kuwa tangu mwezi Mei, vikundi vilivyojihami vimekuwa vikiwalenga watoto katika mashambulizi kwenye vijiji na miji.

Katika visa tofauti kule Bria, Mashariki mwa nchi, wasichana 14 wa umri kati ya miaka 9 na 16 walibakwa katika mapigano ya Mei na Juni, halikadhalika watoto watano wenye umri kati ya miaka miwili na 16 waliuauwa kinyama Bangassou, Kusini Mashariki mwa CAR mnamo Mei walipokuwa wakijaribu kukimbilia nchini DRC.

Wengine 17 walitekwa nyara akiwemo mmoja ambaye tayari ameripotiwa kuuwawa.