Leo ni siku ya ujuzi kwa vijana duniani

16 Julai 2017

Wakati siku ya ujuzi kwa vijana ikiadhimishwa kote duniani , mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating, amesisitiza umuhimu wa kutoa mafunzo ya ufundi stadi na teknolojia kwa vijana nchini Somalia.

Amesema tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana Somalia ni kubwa sana na linatisha , huku kiwango cha chini cha elimu na fursa finyu za ujuzi wa kiufundi na mafunzo ya ufundi ni tatizo kubwa lenye athari mbaya.

Kwa mujibu wa makadirio ya shirika la kazi ulimwenguni ILO, Somalia imeorodheshwa kama moja ya nchi zenye kiwango cha juu zaidi duniani cha ukosefu wa ajira , ikiwa na asilimia 33 tu ya vijana wake walioajiriwa .

Amezitaja sababu kubwa za ukosefu wa ajira kwa vijana nchini humo kuwa ni kutokuwepo uwiano baina ya ujuzi wavulana na wasichana wa Somalia walio nao na mahitaji ya waajiri au ujuzi unaohitajika kuweza kuishi .

Ameongeza kuwa tofauti hiyo siyo tu inaathiri uchumi bali pia kipindi cha mpito kuelekea Somalia iliyojitosheleza, yenye amani, matarajio na jumuishi.

Umoja wa Mataifa hivi sasa unawekeza dola milioni 17.5 katika miradi ambayo inatoa mafunzo ya ujuzi na ufundi kwa vijana wa Somalia , ili kuwapa ujuzi unaohitajika ujuzi wa masuala ya afya, ujenzi, ufundi magari, kilimo, uvuvi na mafunzo ya vitendo.