Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani shambulio kwenye mji wa kale wa Jerusalem

Guterres alaani shambulio kwenye mji wa kale wa Jerusalem

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres amelaani vikali shambulio lililotekelezwa leo asubuhi na washambuliaji watatu kwenye mji wa kale wa Jerusalem na kusababisha vifo vya maafisa wawili wa polisi na kumjeruhi mwingine.

Kupitia taarifa ya msemaji wake, Katibu Mkuu amesema tukio hilo linaweza kuchochea ghasia zaidi na amezitaka pande zote kuchukua hatua stahiki kuzuia kuendelea kwa machafuko.Katibu Mkuu amesema sala na fikra zake ziko na familia za waathirika na amemtakia afueni ya haraka majeruhi.

Guterres amekaribisha pia tamko la kulaani shambulio hilo lililotolewa na Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na hakikisho la waziri mkuu wa Israel Netanyahu Kwamba hali hiyo katika maeneo matakatifu huko Jerusalem itaheshimiwa.

Ameongeza kuwa utakatifu wa maeneo ya kidini unapaswa kuheshimiwa kama maeneo ya kutafakari, sio ya unyanyasaji.