Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa dini wakaa kitako kuzuia mauaji mengine ya kimbari

Viongozi wa dini wakaa kitako kuzuia mauaji mengine ya kimbari

Viongozi wa dini ulimwenguni kote leo hii wamekusanyika hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuanzisha mpango mpya wa utekelezaji wenye lengo la kuzuia mauaji mengine ya kimbari.

Mpango huo ulichukua miaka miwili kuandaliwa na kuongozwa na Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji Mauaji ya Kimbari, Adama Dieng, na una mapendekezo makuu matatu, yenye lengo la "kuzuia, kuimarisha na kujenga,ambayo yatatekelezwa na wadau wote husika ikiwemo viongozi wa dini, asasi za kiraia, serikali za mitaa katika ngazi zote za kitaifa, kikanda na kimataifa.

Akihojiwa na idhaa hii, Bwana Dieng akinukuu kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa mpango huu ni mali ya viongozi wa dini na wadau husika na kwamba Umoja wa Mataifa upo tu kusaidia na kuratibu utekelezaji wake....

(Sauti ya Dieng)

"Naamini kuwa utekelezaji wa mapendekezo haya mapana utachangia sio tu katika kupunguza migogoro lakini pia utachangia katika malengo mengine muhimu, yakijumuisha lengo la kuendeleza amani pamoja na ujenzi wa jamii zenye haki na amani".

Na kuhusu mchango wa viongozi wa dini katika kuzuia mauaji ya kimbari na kuchagiza amani akasema..

(Sauti ya Dieng)

"Sina shaka kuwa wasikilizaji wetu wote watakubaliana nami kuwa viongozi wa dini wanaushawishi mkubwa sana, hebu tafakari wafuasi wao wote, na wakati mwingine wanaushawishi mkubwa zaidi kulioko hata viongozi wa kisiasa, na ndio maana nikahisi katika miaka miwili ambayo tumeanzisha mradi huu kuwa tunahitaji kuwaleta viongozi wa dini."