Teknolojia ya habari na mawasiliano muhimu katika kutimiza SDGs

13 Julai 2017

Wakitanabaisha umuhimu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama) katika ulimwengu wa sasa, ofisi na wakuu wa mashirika zaidi ya 20 ya Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kukumbatia teknolojia hizo ili kuchapusha utekelezaji wa ajenda ya 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu au SDG’s.

Wito huo upo katika ripoti mpya iliyozinduliwa leo mjini Geneva Uswis, ambapo pia maafisa hao wameelezea uhusiano muhimu uliopo baina ya teknolojia ya habari na mawasiliano na malengo 17 ya maendeleo endelevu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akichangia katika ripoti hiyo “ Chapuza mchakato:kumbatia teknolojia kutimiza malengo ya maendeleo” amesema “ Ajenda ya mwaka 2030 inatambua umuhimu wa kuunganishwa na teknolojia kimataifa katika kuchagiza maendeleo ya binadamu.

Ripoti hiyo inatoa ushahidi wa jinsi gani mashirika ya Umoja wa Mataifa yanakumbatia na kwenda sanjari na teknohama , ili kupata manufaa zaidi katika kuzisaidia jamii na watu wenye uhitaji.

Amesema juhudi zinafanyika sasa kuhakikisha mitandao ya mawasiliano na teknohama vinafika maeneo ya vijijini, kutoa mafunzo, kuwapa vifaa na ujuzi mpya wa kidijitali wafanyakazi, na kuhakikisha shule,hospitali, vituo vya afya na miji kwa ujumla inakuwa bora, inajitosheleza kinishati na salama.

Mambo matano muhimu yaliyosisitizwa katika ripoti hiyo ni ni kuhakikisha hakuna nayesalia nyuma, kutambua umuhimu wa teknohamakama chachu ya ubunifu na mabadiliko, kuwapa watu kipaumbele, umuhimu wa hatua za haraka za kukumbatia  teknohama na kuanzisha ubia mpya wa ubunifu.

Naye Katibu mkuu wa muungano wa kimataifa wa mawasiliano ITU, Bwana Houlin Zhao, amesema muungano huo uko tayari kushirikiana na mashirika yote katika kufanikisha azma hii.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter