Wayemen milioni 20 wanategemea hatua za baraza la usalama kusaidiwa

12 Julai 2017

Takriban Wayemeni milioni 20 wanategemea baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua mujarabu ili kusaidia kumaliza vita nchini Yemen ambavyo sasa vimechangia kusambaa kwa kashifa ya kipindupindu.

Akizungumza kwenye kikao cha baraza la usalama hii leo mjini New York Marekani, mkuu wa kuratibu masuala ya kibinadamu wa Umoj wa Mataifa Stephen O’Brien, amesisitiza fedha za ufadhili na msaada zaidi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Watu zaidi ya 1700 wamepoteza maisha kutokana na kipindupindu Yemen na kuna visa vingine 300,000 vinashukiwa kutoka mlangoni mwa wapiganaji walioko ndani na nje.

(SAUTI YA O’BRIEN)

“Kashifa hii ya kipindupindu, imesababishwa na binadamu, na pande hasimu na wale walio nje ya mipaka ya Yemen, ambao wanaongoza, kusaidia, kupigana na kuchagiza hofu na mapigano.”

Ameongeza kuwa watu milioni 7 nchini Yemen wako katika hatari ya baa la njaa wakiwemo watoto milioni 2.3 wa umri wa chini ya miaka mitano, na wengine takriban milioni 16 hawana huduma za kutosha za kujisafi na usafi.

Kwa upande wake mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, akihutubia baraza hilo kwa njia ya video kutoka Jordan amesema, anajitahidi ili kuanzisha upya mazungumzo ya amani na kupata maafikiano ya japo kufikisha msaada zaidi wa kibinadamu na kulipa mishahara ya wafanyakazi wa umma. Kupitia tafsiri ya mkalimani Cheikh amesema viongozi wa kisiasa lazima wasilikilize kilio cha watu wao cha kutaka amani.

(SAUTI YA CHEIKH)

“Hali ya kibinadamu nchini Yemen ni ya kusikitisha, watu wanateseka na vita, njaa na kipindupindu ambacho kimesambaa zaidi katika wiki chache zilizopita, nchi hiyo haikabiliwi na chamngamoto moja bali mlolongo wa zahma ambazo zimeathiri zaidi ya watu milioni 20 na athari hizo zitaendelea hata baada ya vita.”

Naye mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameliambia baraza hilo kwamba watu milioni 15 wanakosa fursa ya huduma za afya za msingi nchini Yemen. Akiongeza kwamba mlipuko wa kipindupindu unashamiri kutokana na kusambaratika mfumo wa afya na kuahidi kwamba WHO itafungua vituo vingine 500 nchini humo.