Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru yaangazia utokomezaji wa silaha za nyuklia

Nuru yaangazia utokomezaji wa silaha za nyuklia

Mkataba wenye nguvu kisheriaa na ambao unalenga kutokomeza kabisa matumizi ya silaha za nyuklia umepitishwa hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Wajumbe kutoka nchi 124 walioshiriki mkutano huo walipiga kura ambapo nchi 122 ziliunga mkono, ilhali Uholanzi ilipinga na Singapore haikuonyesha msimkamo wowote.

Hata hivyo baadhi ya nchi kama vile Marekani, Uingereza, Israel hazikushiriki kabisa kwenye mchakato wa kupatikana kwa mkataba huo zikidai kuwa mkataba huo hautaleta maendeleo yoyote katika kutokomeza silaha za nyuklia ulimwenguni.

Azimio hilo lenye ibara 20 litatiwa saini mwezi Septemba mwaka huu kwenye makao ya Umoja wa Mataifa ambapo nchi zitakazotia saini na kuridhia zitakuwa zimekubali kutekeleza mambo kadhaa.

Mathalani katika ibara ya Nne inataka nchi mwanachama wa mkataba huu ambaye alikuwa anamiliki silaha za kemikali akubali taasisi yenye uwezo ikague na kuthibitisha kuwa imeondokana nazo.

Balozi Elayne Whyte Gómez kutoka Costa Rica ni mwenyekiti wa mkutano huo uliowezesha kupatikana kwa mkataba..

(Sauti ya Balozi Elayne)

“Mkataba ambao tumepitisha siyo tu kwamba umekidhi mamlaka ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya kuweka maadili yanayoiamrisha na kusaidia muundo wa kudhibiti kuenea kwa silaha, bali pia umegusa wengi matarajio ya wengi waliokuwepo kwenye mkutano huu hasa mashirika ya kiraia. Na hili ndio napenda kusisitiza kuwa ufahamu wa mashirika haya na mashinikizo yao kwa miongo yote ya kuona jamii ya kimataifa isonge mbele katika kupiga marufuku silaha za nyuklia.”