Myanmar isake suluhu kwa wasio na utaifa- Grandi

6 Julai 2017

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi amehitimisha ziara yake ya kwanza nchini Myanmar kwa kutoa wito kwa nchi hiyo kusaka suluhu ya endelevu na shirikishi juu ya suala la watu wasio na utaifa.

Ametoa wito huo baada kutembelea maeneo ya Yangon, Naypyitaw pamoja na Sittwe na Maungdaw kwenye jimbo la Rakhine.

Bwana Grandi amenukuliwa kupitia taarifa iliyotolewa na UNHCR akisema kuwa alikuwa na mazungumzo na viongozi wa serikali akiwemo Mshauri Mkuu wa serikali ya Myanmar Aung San Suu Kyi ambao wamemhakikishia kuwa wakimbizi walioko Thailand wanaruhusiwa kurejea nyumbani.

Hata hivyo Bwana Grandi amesema wamekubaliana kuwa kurejea huko kuwe kwa hiari na kwamba wakirejea wawekewe mazingira ya kujitegemea badala ya kuendelea kuwa tegemezi.

Amesema wamejadili pia suala la kufikisha misaada ya kibinadamu kwenye majimbo ya Kachin na Rakhine ambako jumla ya watu 220,000 kwenye majimbo hayo wamekuwa wakiishi kwenye kambi kwa zaidi ya miaka mitano sasa kutokana na ghasia dhidi ya makundi ya kidini.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter