Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM watoa wito wa kusitishwa kunyongwa kwa Morva

Wataalam wa UM watoa wito wa kusitishwa kunyongwa kwa Morva

Hukumu ya kifo ya mwanamume anayesubiri kunyongwa jimbo la Virginia nchini Marekani inapaswa kusitishwa kwa kuzingatia ulemavu wake wa akili, wamesema wataalam wa haki wa Umoja wa Mataifa Jumatano.

Katika ombi lao kwa mamlaka, wataalamu hao Agnes Callamard na Danius Puras wamesema hali ya kiakili ya mwanamume huyo William Morva raia wa Hungary, haikuwekwa bayana wakati kesi yake ikiendeshwa.

Morva anatarajiwa kunyongwa kesho Alhamisi ya Julai 6 kufuatia hukumu yake yam waka 2008 ya mauaji ya mlinzi wa hospitali na naibu afisa wa usalama.

Ulemavu wa Morva uligunduliwa mwaka 2014, ambapo kwa mujibu wa mtaalamu wa afya ya akili aliyeteuliwa na mahakama, huenda ulemavu huo ndio ulichochea kosa lake.

Wataalam hao wameelezea kusikitishwa kwao na hali inayozidi kuzorota ya mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 35 na kutolea wito gavana wa Virginia kuruhusu kesi hiyo kusikilizwa upya.

Wataalam hao wanaohusika na mauaji holela,  halaiki na kunyongwa na afya ya mwili na akili wamesema kwamba hali ilivyo sasa ni kwamba mawasiliano kati ya timu ya kisheria na bwana Morva yamesitishwa na hivyo kukandamiza juhudi zao za kutetea kesi huku siku ya kunyongwa ikibisha hodi.