Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko thabiti ya UM yahitajika kukidhi SDGs- Guterres

Mabadiliko thabiti ya UM yahitajika kukidhi SDGs- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwasilisha ripoti ya mapendekezo yake kuhusu mabadiliko ya mfumo wa Umoja wa Mataifa. (Picha: UN/Kim Haughton)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo amewasilisha ripoti yake inayopendekeza mabadiliko makubwa ya muundo wa utendaji wa chombo hicho ili kiweze kutekeleza kwa ufanisi ajedna ya maendeleo endelevu, SDGs.

Akiwasilisha ripoti hiyo ya kurasa 24 mbele ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo, Bwana Guterres amesema chombo hicho hivi sasa kipo katika mfumo ambamo kwao kasi yake si ya kuweza kufanikisha SDGs.

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (katikati) akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed kabla ya kuwasilisha ripoti. (Picha:UN/Kim Haughton)
Amesema iwapo mambo yatasalia kama yalivyo hivi sasa itakuwa vigumu kukidhi mahitaji ya wananchi wanaotarajia kunufaika na ajenda 2030 yenye malengo 17 ikiwemo kutokomeza umaskini na njaa.

(Sauti ya Guterres)

“Nyote mlikuwa makini katika kuandaa ajenda 2030 ya kutokomeza umaskini, kulinda mazingira ya sayari yetu, ajenda yenye matarajio makubwa zaidi kuwahi kupitishwa na Umoja wa Mataifa. Lakini mnafahamu kuwa mfumo uliopo haufanyi kazi ipasavyo.”

Hivyo Bwana Guterres ametaja miongozo mikuu minane ya mabadiliko hayo ikiwemo mosi kubadilika kutoka mfumo wa utekelezaji malengo ya milenia hadi utekelezaji wa SDGs akisema..

(Sauti ya Guterres)

“Kwa sasa mfumo uliopo una mapengo makubwa kwa upande wa stadi na mifumo. Mfumo uliopo bado unatekeleza malengo machache yaliyojikita kwenye sekta badala ya kuwa mtambuka na kujumuisha ajenda ya maendeleo endelevu.”

Mapendekezo mengine ni kubadilisha mfumo wa utendaji wa timu za Umoja wa Mataifa katika kila nchi ili utendaji wake uendane na mahitaji huku akisema kuwa mabadiliko hayatakuwa rahisi na kwamba..

(Sauti ya Guterres)

"Jaribio thabiti la marekebisho si kupimwa kwa maneno New York au Geneva. Yatapishwa kupitia matokeo ya maisha ya watu ambao tunawahudumia.”

Katibu Mkuu amesema mapendekezo ya kina yatawasilishwa kwa kila nchi mwanachama ifikapo mwezi Disemba kwa lengo la kusaidia nchi hizo kufanikisha SDGs ifikapo mwaka 2030.