Mjumbe mpya wa UM Burundi akutana na Rais Nkurunziza

30 Juni 2017

Mjumbe mpya maalumu wa katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Burundi Michel Kafando amefanya ziara nchini humo kujitambulisha katika jukumu lake la kusaidia kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo. Kuangazia ziara hiyo hii hapa ni ripoti ya mwandishi wetu wa Maziwa Makuu Ramadhani Kibuga akiripoti kutoka Bujumbura.

(Taarifa ya Kibuga)

Bwana Michel Kafando amekuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Rais Pierre Nkurunzizana kutangaza azma ya majukumu yake mpya.

“Nimemueleza rais ni njia zipi na kwenda kushughulikia wajibu wangu kama mjumbe maalumu. Pia Malengo yangu ambayo napanga kutekeleza. Niko tayari kutafuta suluhu ya mgogoro wa Burundi.”

Mwanadiplomasia kutoka Burkina Faso anakuja kusimamia Umoja wa mataifa burundi katika mazingira magumu baada ya watangulizi wake Said Djinit, Abdoulaye Bathily na Jamal Ben Omar, wote kulaumiwa na kukataliwa na serikali ya burundi kwa madi ya kuegemia upande wa upinzani. Hata hivyo Michel Kafando amesema anaamini atafaanikisha wajibu wake licha ya uzito wa kazi hiyo.

“Kutafuta amani ni mapambano makubwa. Ni kweli watangulizi wangu wakati fulani walijikuta wakimaliza kazi zao katika mazingira magumu. Kila mtu ana uzoefu wake .Siwezi sema kuwa nina fimbo ya miujiza. Ni kweli jukumu langu ni ligumu. Lakini Nitajaaribu kuweka juhudi na bidii inayostahili. Ninaamini kuna haja ya kufanya kazi kwa kutilia maanani muafaka na maelewano na nchi husika yaani Burundi.”

Bwana Kafando, Rais wa zamani wa Burkinafaso aliteuliwa mwezi uliopita kuwa Mjumbe maalumu wa katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Burundi katika juhuzi za kumaliza mgogoro wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili na kusababisha watu zaidi ya 500 kuuwawa huku raia zaidi ya laki nne wakilazimika kuchukua hifadhi ugenini.

Baada ya mazungumzo na mamlaka Burundi na wanadiplomasia, mjumbe huyo atakuwa na mazungumzo na wapatanishi wa mzozo wa Burundi Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa pamoja na Viongozi wa Muungano wa Afrika.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter