Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 50 ya kukaliwa Palestina bado hakuna suluhu

Miaka 50 ya kukaliwa Palestina bado hakuna suluhu

Katika kuadhimisha miaka 50 ya Israel kukalia eneo la Wapalestina tangu 1967, kamati ya utekelezaji wa haki zisizo na mjadala za watu wa Palestina imeandaa mkutano wa siku mbili kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa leo na kesho Ijumaa ili kutathimini jinsi ya kumaliza ukaliaji huo wa Israel.

Jukwaa hilo lililoandaliwa kwa mujibu wa maazimio ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa nambari 71/20 na 71/21 linajikita katika njia ya kuelekea uhuru wa Palestina, haki na amani kwa watu wa Palestina, lakini pia kuweka mazingira bora kwa aili ya haki za binadamu, maendeleo na amani ya kudumu.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohamed amewasilisha ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwenye jukwaa hilo akisema

(SAUTI YA AMINA1)

“ukaliwaji umeleta mzigo mkubwa wa kibinadamu na maendeleo kwa watu wa Palestina, vizazi vya Kipalestina vimekuwa katika makambi za wakimbizi zenye msongamano, wengi katika umasikini huku wakiwa hawana au wana matumaini kidogo sana kwa mustakhbali wa watoto wao. Miaka 50 ya kukaliwa imezusha mzunguko wa machafuko na chuki na kutuma ujumbe wa kimakosa kwa Wapalestina kwamba ndoto zao za kuwa na taifa huenda zisitimie, na kutuma ujumbe kwa Waisrael kwamba matamanio yao ya amani, usalama na kutambuliwa kikanda hayawezi kutimia.”

Na kwa mukhtada huo ameongeza

(SAUTI YA AMINA2)

“Kumaliza ukaliwaji huo ndio njia pekee ya kuweka msingi wa kupata amani ambayo inakidhi mahitaji ya Israel na matarajio ya Palestina yakuwa na taifa na uhuru. Ndio njia pekee ya kupata haki zisizotekelezwa za Wapalestina , ni wakati wa kumaliza vita kwa kuanzisha taifa huru la Palestina litakalokuwa sanjari na kwa amani na usalama na Israel. Kutatua mzozo baina ya Isarel na Palestina kutaondoa chanzo cha ghasia za itikadi kali na ugaidi Mashariki ya Kati na kufungua milango ya ushirikiano, usalama, mafanikio na haki za binadamu kwa wote.”