Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 6 DRC hawana uhakika wa kupata mlo- FAO

Watu milioni 6 DRC hawana uhakika wa kupata mlo- FAO

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hali ya chakula inaelezwa kuwa ni mbaya kwenye maeneo ya Kasai, Kivu na Tanganyika huku watu milioni Sita nchini humo wakiripotiwa kuhitaji msaada wa haraka. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC licha ya mzozo wa wenyewe kwa wenyewe kwenye maeneo ya Kasai, Kivu na Tanganyika, migogoro inayoendelea nchi jirani za Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR imemiminisha wakimbizi.

Mazingira ya sasa yamesababisha watu milioni 6 kukosa uhakika wa chakula kwa kuwa hawawezi kuendelea na shughuli za kujipatia kipato.

Luca Ruso, afisa mwadamizi wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO ambaye hivi karibuni ametembelea maeneo hayo anaeleza walichoshuhudia..

(Sauti ya Luca)

“Kwa upande mmoja mtu una janga la kiuchumi na hapo hapo ni mkimbizi wa ndani. Wengi wao hawajavuna kwa misimu mitatu ya kilimo. Hii imeathiri sana hali ya chakula na wamehamia kambi za wakimbizi wa ndani. Wana hamu ya kurejea nyumbani kwani kambini ni mazingira ya muda. Hata hivyo wana hofu kutokana na kumbukumbu za ghasia ambazo walizipitia.”

Bwana Russo ameomba jamii ya kimataifa isisahau mzozo unaoendelea DRC kwani linaathiri maisha ya watu na kwamba usaidizi uwezeshe wananchi kurejea katika maisha ya kawaida ikiwemo shughuli za kujipatia kipato.