Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia waliokwama Al-Raqqa wanahitaji ulinzi haraka

Raia waliokwama Al-Raqqa wanahitaji ulinzi haraka

[caption id="attachment_321798" align="aligncenter" width="625"]hapanapaleal-raqqa

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein leo ameelezea hofu yake kuhusu hatma ya raia waliojikuta katikati ya mashambulizi ya kupinga ISIL mjini Al-Raqqa, Syria ambako watu takribani 100,000 wamekwama kutokana na kushika kasi kwa mashambulizi ya anga na ardhini.

Idadi ya vifo na majeruhi ambao ni raia imeendelea kuripotiwa huku njia nyingi za watu kutoroka zikifungwa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa angalau raia 173 wameuawa na mashambulizi ya anga tangu Juni Mosi, haya yakiwa ni makadirio tu huenda idadi kamili ikawa kubwa zaidi.

Japokuwa baadhi ya watu wamefanikiwa kukimbia baada ya kuwalipa wasafirishaji haramu kiwango kikubwa cha fedha bado kuna taarifa za ISIL kuzuia raia kukimbia machafuko.

Zeid ametoa wito kwa pande zote katika mzozo kuweka hatua ambazo zitaruhusu raia wanaotaka kukimbia mapigano kufanya hivyo katika hali salama.