Wahamiaji 52 wafa jangwani Sahara:IOM

Wahamiaji 52 wafa jangwani Sahara:IOM

Wahamiaji 52 wafa jangwani Niger wakati operesheni ya uokozi ya shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM ikifanikiwa kuwanusuru wengine 600 waliokwama Jangwa la Sahara.

Kwa mujibu wa shirika hilo Jumapili asubuhi Juni 25 wahamiaji 24 waliuarifu uongozi wa Niger kwamba wamekwama jangwani ingawa haijafahamika walikuwa wametembea kwa muda gani katika jangwa hilo la Niger ya Kati.

Waliokewa walipelekwa Seguedine lakini mmoja alipoteza maisha walipowasili. Miongoni mwa waliokolewa ni pamoja na raia wa Gambia, Nigeria, Senegal na Cote divoire.

Watu hao walikuwa wakisafiri katika kundi la watu 75 kwenye magari ma tatu walipotelekezwa jangwani na wasafirishaji haramu.

Uongozi wa Niger umejaribu kuwasaka wahamiaji 51 wengine bila mafanikio kutokana na kimbunga cha mchanga na wanahofia wamepoteza maisha. Hadi sasa IOM imeshawaokoa wahamiaji 600 waliokuwa wamekwama katika janga la Sahara.