Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 5.6 ziwa Chad wamo hatarini

Watoto milioni 5.6 ziwa Chad wamo hatarini

Zaidi ya watoto milioni 5.6 wako hatarini kupata magonjwa yatokanayo na maji machafu wakati msimu wa mvua ukinyemelea eneo la ziwa Chad, limesema leo Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF.

Ukosefu wa usalama kutokana na migogoro katika ukanda huo pamoja na janga la kibinadamu linalosababishwa na kundi la kigaidi la Boko Haram linahatarisha zaidi hali hii, mafuriko na matope barabarani yakitarajiwa kuzorotesha ufikishaji wa misaada ya kibinaadamu mashinani.

UNICEF na wadau wengine wamo mbioni kutoa mafunzo kwa jamii katika eneo hilo kuhusu madhara ya ugonjwa wa kipindupindu na hatua za kujiepusha na maambukizi, na pia kuandaa vifaa maalum na dawa katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi Niger, Cameroon na Chad.