UNESCO yalaani uharibifu wa mnara wa Al Hadba na msikiti wa Al Nuree Mosul

22 Juni 2017

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO, Irina Bokova, amelaani uharibifu uliofanywa kwenye msikiti wa Al Nuree na mnara wa Al Hadba Minaret mjini Mosul nchini Iraq.

Amesema msikiti na mnara huo ni miongoni mwa maeneo ya urithi ya mji wa Mosul na yalikuwa kama ishara ya utambulisho, uimara na mali.

UNESCO inasema wakati kundi la kigaidi la Daesh lilipolenga msikiti na mnara huo miezi michache iliyopita watu wa Mosul walijipanga mduara kulinda maeneo hayo, wakidhihirisha kwa mara nyingine kwamba kulinda maeneo ya urithi wa kitamaduni hauwezi kutenganishwa na ulinzi wa maisha ya watu.

Bi Bokova amesema uharibifu huu mpya unatonesha vidonda vya jamii ambayo tayari inaghubikwa na janga la kibinadamu la vita vilivyosababisha watu milioni 3 kuwa wakimbizi wa ndani na wengine milioni 6.2 kuhitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.

Tangu kuanza kwa operesheni ya Mosul Oktoba 2017 takriban watu 75,000 hadi 800,000 wametawanywa na machafuko mjini Mosul na wengi wamekwama au wanatumiwa kama ngao vitani.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter