Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafadhili wajitumbukize hatarini nasi kuokoa maisha

Wafadhili wajitumbukize hatarini nasi kuokoa maisha

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo inasema kinachoshangaza na kushtua ni kwamba kuna mamia ya mashirika ya kibinadamu ya kutoa misaada katika maeneo yaliyoathirika na majanga ya asili lakini ni dazani moja tu yenye uwezo wa kutoa msaada katika maeneo hatari ya kivita ambayo kwayo watoto, wanawake na majeruhi wanauhitaji zaidi.

Akiwasilisha ripoti hiyo iitwayo  “Uwepo na Upeo: Kukaa na Kufikisha misaada, Miaka mitano ijayo” mbele ya waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi leo, Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, Stephen Obrien amesema mabadiliko katika hali ya migogoro, mashambulizi dhidi ya watoa misaada, ukosefu wa fedha na uwezo wa usimamizi wa hatari yamelazimu mashirika mengi kushindwa kutumikia jamii zinazoathiriwa na machafuko na migogoro.

Akiongoza utafiti huo Mshauri Maalumu wa Umoja wa Mataifa Jan Egeland amesema wale ambao wanashindwa kuwasaidia ni wahudumu wa misaada wa kitaifa ambao wamo hatarini zaidi kuliko wale wa kimataifa na kinachotakiwa sasa ..

(Sauti ya Egaland)

“ Ni kuleta mashirika mengi zaidi kwenye uwanja wa mapambano, ili kuwafikia na watu wanaotuhitaji zaidi, na ili kufanya hivyo, tunahitaji ushirikiano thabiti zaidi na wafadhili, wanatakiwa kuwepo nasi ,kuwekeza katika usimamizi wa hatari, na katika jitihada za usalama zinazohitajika”.