Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiwango cha madhila kwa watu wa Syria kinaendelea kutia hofu-Guterres

Kiwango cha madhila kwa watu wa Syria kinaendelea kutia hofu-Guterres

Ninaendelea kushangazwa sana na kusikitishwa na kina cha mateso ya nayowaghibika watu wa Syria. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akionya kwamba maisha ya kila siku kwa mamilioni ya watu yako hatarini.

Kupitia taarifa ya msemaji wake Guterres amesema raia wanaendelea kuuawa, kujeruhiwa na kutawanywa katika kiwango cha kutisha, na kinachomtia hofu zaidi ni maeneo ambayo watu hao wanapata usalama kama hospitali na shule yanaendelea kulengwa na mashambulizi.

Ameongeza kuwa maeneo yanatia hofu zaidi ni Raqqa ambako raia wamekwama na wanakabiliwa na vitisho kutoka kila upande. Katibu Mkuu ametoa wito kwa wanaondesha operesheni za kijeshi nchini Syria kufanya kila liwezekanalo ndani ya uwezo wao kuwalinda raia na miundombinu wakati huu mapigano yakiendelea Raqqa na kwingineko.

Pia amesema ni muhimu kwa pande zote kuhakikisha misaada ya kuokoa maisha inawafikia wanaoihitaji haraka iwezekanavyo.